Tuesday, April 23, 2013

Afande Selle: Siifikirii Siasa

Afande Selle
MWANAMUZIKI wa Mziki wa Kizazi Kipya kwenye miondoka ya Hip Hop, Selemani Msindi maarufu kama Afande Selle ametanabaisha juu ya msimamo wake kuhusiana na masuala ya kisiasa.
Afande ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wake mpya uitwao Dini Tumeletewa, ameyasema hayo nilipokuwa nafanya mahojiano naye kwenye kipindi cha The Takeover kinachoruka hewani kila siku za wiki saa nane mpaka kumi jioni ndani ya TBC fm.

Katika mahojiano hayo nilimuuliza Afande juu ya jamii kumuhusisha na kujikita na mambo ya kisiasa alijibu na kusema “sio mbaya kwa jamii kufikiria hivyo, mwanasiasa ni mtu wa aina gani? Ni mtu ambae ana uzalendo kwa taifa lake, analijua taifa lake na analipigania kuliokoa.
Mimi binafsi sijaitoa nyimbo hiyo kwa ajili ya kwamba nataka niwe Mbunge au nani, isipokuwa ni mapenzi yangu mema kwa Taifa langu na ni kutokana na hali halisi ambayo ipo sasa, hivi unaiona mwenyewe inafikia muda watanzania wanapigana kwa ajili ya kuchinja tu, kitu ambacho hatujakizoea, watanzania wanagombana kwa sababu ya tofauti zao za majina”.
Aliendelea na kuongeza “Kwa hiyo mtu anaweza kufikiria mengi kwa sababu nimetumia akili ambayo pengine wananiona kama ni mtu ambaye kitu ambacho nimekisema anatakiwa pengine akifanye Raisi au akifanya Mbunge, lakini nimekifanya mimi ambae ni raia wa kawaida, si kwa ajili ya siasa, ni kwa ajili ya uzalendo wangu na taifa langu, siasa ni kitu ambacho kipo pembeni na maisha yangu, sifikirii kwa sasa hivi".
Watu wengi wamekuwa wakimuhusisha Afande Selle na masuala ya kisiasa, huku wakisema kwamba msanii hiyo ana nia ya kugombea Ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.

No comments:

Post a Comment