Thursday, April 25, 2013

Leo Ni Siku ya Malaria Duniani


Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Malaria Duniani ifikapo kila mwaka tarehe 25 Aprili. Siku hii ilianzishwa kunako mwaka 2007 ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita imejitahidi kupambana na ugonjwa wa Malaria duniani.
Tangu mwaka 2000 kiwango cha vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Malaria kimepungua kwa asilimia 25%. Kuna nchi 50 kati ya nchi 99 zinazoendelea kufanya vyema ili kufikia Malengo ya Maendeleo ya Millenia kwa mwaka 2015 kwa kupunguza vifo kwa asilimia 75%. Jambo hili linawezekana ikiwa kama kutakuwepo na udhibiti zaidi wa ugonjwa wa Malaria, kwa kuwa na vifaa vizuri vya kuchunguza pamoja na dawa zinazotibu Malaria.

Malaria ni ugonjwa unaoendelea kupukutisha maisha ya watu wapatao 660,000 kutoka kila kona ya dunia, wengi wao ni watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanaoishi Kusini mwa Jangwa na Sahara.

Zaidi ya watu millioni 200 wanashambuliwa na ugonjwa wa Malaria. Kesi nyingi hazipimwi wala kupatiwa tiba muafaka. Dawa zisizo na viwango zinasababisha usugu, jambo ambalo linaweza kukwamisha jitihada za Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria.

Kauli mbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani kwa Mwaka 2013; Wekeza kwa siku za baadaye. Shinda Malaria.

No comments:

Post a Comment