Thursday, December 12, 2013

Kamati Yampa Suarez Goli la Nne Kwenye Ushindi wa Liverpool wa 4-1 Dhidi ya West Ham


Kamati ya magoli Chama cha Soka nchini Uingereza imeamua kumpa mshambuliaji wa Liverpool, Luis Suarez, goli ambalo awali lilihesabika ni la kujifunga kwenye mchezo dhidi ya West Ham, hivyo kumfanya mchezaji huyo kuongeza idadi ya magoli aliyofunga na kufikia 15.

Suarez amepewa goli la nne kwenye mechi ambayo Liverpool ilishinda 4-1 dhidi ya West Ham Jumamosi iliyopita, goli ambalo awali lilihesabika ni la kujifunga na mlinzi wa Hammers, Joey O’Brien.

Goli hilo lililofungwa dakika ya 84 lilikuja wakati Suarez alipopiga mpira kutoka mbali na shuti lake lilibadilisha uelekeo baada ya kumgonga O’Brien, ukimuacha kipa Jussi Jaaskelainen akiwa hana namna.

Kamati imeamua Suarez anastahili kupewa goli hivyo sasa anakuwa na jumla ya magoli 15 kwa mechi 10 za ligi alizocheza, huku akiwa amezikosa mechi tano za mwanzo wa msimu katika kipindi ambacho alikuwa akitumikia adhabu ya kufungiwa mechi 10 mara baada ya kumng'ata mlinzi wa timu ya Chelsea Branislav Ivanovic msimu uliopita.

Mchezji wa Manchester City, Sergio Aguero, kwa sasa yupo nyuma ya Suarez kwa magoli matatu kwenye chati ya ufungaji wa magoli wa ligi hiyo, akiwa amefunga magoli 12 kwenye mechi 14.

No comments:

Post a Comment